1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani, China zafanya mazungumzo ya ngazi ya juu

Bruce Amani
20 Juni 2023

Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz na Waziri Mkuu wa China Li Qianq wanakutana katika mazungumzo mjini Berlin yatakayojikita kwenye mada za biashara, mabadiliko ya tabia nchi na vita vya Urusi nchini Ukraine.

https://p.dw.com/p/4SoH2
Deutschland-Besuch der chinesischen Regierung
Picha: Markus Schreiber/AP/picture alliance

Mkutano huo wa mjini Berlin ni mara ya saba kwa Ujerumani na China kufanya mazungumzo ya ngazi ya juu na unajiri siku moja baada ya Rais wa China Xi Jinping kukutana na Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Marekani Antony Blinken, kuashiria juhudi za Beijing kuzijongelea nchi za Magharibi na kuimarisha mahusiano yaliyoingia doa.

Li, katibu wa zamani wa Chama cha Kikomunisti katika mji wa Shanghai ambaye aliingia madarakani kama afisa wa pili mkuu wa China, alikutana jana na Rais wa Ujerumani Frank Walter Steinmeier na kuwa na chakula cha jioni na Scholz katika makao makuu ya kansela kabla ya kuanza mazungumzo rasmi

Deutsch-chinesische Regierungskonsultationen
Ujerumani, China watafanya mazungumzo ya ngazi ya juuPicha: Michael Kappeler/dpa/picture alliance

Kansela wa Ujerumani Scholz ametangaza kuwa kundi la Nchi saba tajiri ulimwenguni G7 zinatafakari kutafuta uwiano mzuri kati ya biashara na China na utegemezi wa mauzo ya nje ya nchi hiyo "G7 haina nia ya kuzuia kupanda kwa uchumi wa China, na wakati huo huo tunafuatilia kwa karibu kuepusha utegemezi hatari wa kiuchumi."

Ujerumani ina nia ya kudumisha uhusiano mzuri na China, mshirika wake mkuu wa kibiashara, licha ya wasiwasi kuhusu kuongezeka kwa uthubutu wa Beijing na kukataa kwake kukosoa uvamizi wa Urusi nchini Ukraine.

Scholz alisema anataka kuepuka utegemezi mkubwa kwa biashara ya China na kutanua usambazaji wa bidhaa muhimu za Ujerumani – mbinu aliyoiita "kuondoa hatari" wakati akipinga wazo la "kujitenga" na China.

Waziri wa mambo ya kigeni wa China Qin Gang hatoshiriki mazungumzo ya leo mjini Berlin. Alilazimika kubaki nyumbani kufuatia ziara ya Blinken mjini Beijing. Scholz aliisifia ziara hiyo lakini akasema bado kuna tofauti kati yao na China. "Na ukweli kuwa Waziri wa mambo ya nje wa Marekani alikuwa China ni dalili nzuri ya hatua inayohitajika sana ya kurejesha uhusiano. Hii haimaanishi kuwa hakuna masuala yoyote ya kujadiliwa, kwamba hakuna tofauti za mitazamo, ambazo ni za wazi."

China | US Außenminister Blinken in China
Waziri Blinken alikutana na Rais Jinping mjini BeijingPicha: Li Xueren/Xinhua/IMAGO

Mkakati mpya wa usalama wa kitaifa uliochapishwa karibuni na Ujerumani unaielezea China kuwa ni „"mshirika, mshindani na mpinzani wa kimfumo."

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya nje wa China Wang Wengbin alisema wiki iliyopita kuwa chaguo la Ujerumani kuwa kituo cha kwanza cha ziara ya Li "linaonyesha umuhimu mkubwa ambao China inauweka kwenye mahusiano ya China na Ujerumani.”

Baada ya kulitembelea taifa kubwa kabisa kiuchumi katika Umoja wa Ulaya, Li ataelekea Ufaransa, taifa la pili kubwa kiuchumi, ambako atahudhuria "Mkutano wa Kilele wa Mkataba Mpya wa Ufadhili Ulimwenguni.” Mkutano huo unaandaliwa chini ya mpango ulioanzishwa na Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron.

AFP, Reuters, DPA, AP